Header Ads

test

POLISI SABA WAUAWA KWA RISASI MKOA WA PWANI




Askari saba wa jeshi la polisi waliokuwa katika doria kijiji cha Jaribu mpakani mwa wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani nchini Tanzania waliuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi majira ya saa 12 jioni Aprili 13, 2017.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia tukio hilo kwani ni mapema sana. Aliwasihi waandishi kumuacha kwanza hadi hapo taarifa rasmi itakapoandaliwa ataweza kuujulisha umma kuhusu yale yote yaliyotokea.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mwigulu Nchemba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo licha ya kusema kuwa hana taarifa za kutosha juu ya tukio zima hadi hapo atakapowasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu. Lakini aliahidi kuwa watu hao watatafutwa popote pale walipo na hatua dhidi yao zitachukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo.

Pia Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania IGP Ernest Mangu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa za awali zinadai kuwa polisi hao walikuwa kwenye gari wakirejea kituoni kutoka kwenye doria na walishambuliwa na watu waliotokea msituni na dereva wa gari la polisi alipigwa risasi na kupoteza uwezo wa kuongoza gari na kisha askari wengine waliokuwepo wakashambuliwa. Askari mmoja aliyejeruhiwa amelazwa katika Hospitali ya Mchukwi.



Tangaza Nasi kupitia [dawatihurutz.blogspot.com]

No comments